Home ยป Vijana wabunifu wahimizwa kuchangamkia bilioni 4.6 za mitaji walizotengewa

Vijana wabunifu wahimizwa kuchangamkia bilioni 4.6 za mitaji walizotengewa

by Joshua Kiziba

Vijana wabunifu wametakiwa kujitokeza na kuchangamkia fursa za mitaji na mafunzo zinazotolewa ili waweze kugeuza mawazo yao kuwa biashara endelevu na chanzo cha ajira.

Wito huo umetolewa kufuatia serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutenga shilingi bilioni 2.3 kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu kwa ajili ya kutoa mitaji wezeshi kwa njia ya mikopo nafuu kwa wabunifu wanaofika hatua ya kupeleka sokoni bidhaa au huduma zitokanazo na ubunifu wao.

Aidha, baadaye Benki ya CRDB iliwekeza shilingi bilioni 2.3 katika mfuko huo na kufanya mtaji wa kuwezesha wabunifu kuwa na jumla ya shilingi bilioni 4.6.

Licha ya uwekezaji huo, mwamko wa vijana umekuwa mdogo ambapo katika kipindi cha miezi 10, vijana saba tu ndio wamenufaika na mfuko wa huo, ambapo baadhi ya waombaji hawakukidhi vigezo vya kupata mitaji hiyo.

Kati ya shilingi bilioni 4.6 zilizotolewa, shilingi milioni 767 pekee ndiyo zimechukuliwa, na hivyo vijana wamehimizwa kutumia fedha hizo kubali mawazo yao kuwa bidhaa na huduma ambazo zitatoa mchango kwa maendeleo ya jamii na kukuza uchumi.