Home » Wananchi 20,000 wa Bukombe kunufaika na ajira mradi wa madini

Wananchi 20,000 wa Bukombe kunufaika na ajira mradi wa madini

by Joshua Kiziba

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wanatarajiwa kunufaika na ajira takribani 20,000 pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na uwekezaji unaotarajiwa kuanza katika eneo la madini ya dhahabu Kigosi.

Mradi huo pia unatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali pamoja na kuleta teknolojia ya kisasa katika sekta ya madini.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa uwekezaji kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kampuni ya Plantcor Mining and Plant Hire (Pty) Ltd, Naibu Waziri wa Madini Dk. Steven Kiruswa amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuendeleza rasilimali za madini na kukuza uchumi wa taifa.

“Mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa ubia. STAMICO, kwa niaba ya serikali ya Tanzania, itashiriki katika hatua zote muhimu kuanzia utafiti wa kina wa madini, uendelezaji wa mgodi hadi uzalishaji.

“Muundo huo unalenga kulinda maslahi ya taifa huku ukiwezesha upatikanaji wa teknolojia na utaalamu wa kisasa kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa,” amesema Dk. Kiruswa.