Home ยป Rais Samia kuteuliwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto

Rais Samia kuteuliwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto

by Joshua Kiziba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo kuelekea Addis Ababa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika tarehe 14 hadi 15 Februari, 2026.

Kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu, tarehe 13 Februari 2026, Rais Samia anatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), utakaofanyika chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Samoei Ruto, na baadaye kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed Ali.

Rais Dkt. Samia pia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Mhe. Russell Mmiso Dlamini; Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assoumani; Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed; pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (Afl)B), Dkt. Sidi Ould Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na maendeleo.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika utafunguliwa rasmi tarehe 14 Februari 2026, na utaongozwa na Kaulimbiu ya Mwaka 2026 inayosema: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Huduma Salama za usafi wa Mazingira ili Kufikia Malengo ya Ajenda 2063.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza hatua za pamoja za bara katika kuhakikisha usalama wa rasilimali maji, afya ya jamii, na maendeleo endelevu.

Tanzania inakamilisha muda wake wa kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika baada ya kulitumikia kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, hivyo kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, utulivu na usalama barani Afrika.

Sambamba na masuala mengine, Mkutano huo utatangaza rasmi uongozi wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026, ambapo Jamhuri ya Burundi itachukua nafasi ya Uenyekiti wa Umoja huo, huku Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, ikiwakilisha Kanda ya Mashariki, nafasi inayoakisi imani ya Nchi Wanachama kwa mchango na uongozi wa Tanzania katika masuala ya Bara la Afrika.

Aidha, katika Mkutano wa mwaka huu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amependekezwa kuteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, uteuzi ambao unatarajiwa kupitishwa rasmi na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Uteuzi huo unaakisi dhamira ya Tanzania katika kuimarisha huduma za afya, ustawi wa familia, na maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika.

Kupitia ushiriki wake katika Mkutano huu, Tanzania inalenga kuendelea kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda na kimataifa, kutetea maslahi ya taifa, na kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Afrika yenye amani, mshikamano, uthabiti wa kiuchumi na maendeleo endelevu.