Serikali yapunguza ada za leseni kwa waandaa maudhui mitandaoni kwa zaidi ya asilimia 80

by Joshua Kiziba

Serikali imepunguza ada za leseni kwa watoa na wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kupanua wigo wa ushiriki, kuhamasisha ubunifu wa kidijitali na kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi katika sekta ya habari.

Ada ya leseni kwa watoa maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi shilingi 50,000, huku ada ya maombi ikiwa shilingi 10,000.

Kwa upande wa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepunguzwa kutoka shilingi milioni 1 hadi shilingi 100,000, na ada ya maombi kuwa shilingi 20,000 tu.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wabunifu wa maudhui ya ndani.

Aidha, serikali imedhamiria kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa vyombo vya habari, huku ikisisitiza ubora wa maudhui, kuzingatia maadili ya taaluma na kulinda haki miliki.