Home » Mtunzi wa wimbo wa ‘Tanzania Yetu,’ Mzee Hiza afariki dunia

Mtunzi wa wimbo wa ‘Tanzania Yetu,’ Mzee Hiza afariki dunia

by Joshua Kiziba

Nguli wa muziki nchini Tanzania na mtunzi wa wimbo maarufu wa Tanzania Yetu, Mzee Steven Hiza amefariki dunia Februari 16 mwaka huu.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa Rhumba Tanzania, Hassan Msumari imeeleza kuwa Mzee Hiza alifariki jana jioni Mwanzange, Tanga na kwamba taarifa za mazishi zitatolewa.

Mzee Hiza, ambaye alikuwa na Atomic Jazz Band, anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki wa kizalendo, hususan kupitia wimbo huo uliotungwa takribani miaka 60 iliyopita na ambao umeendelea kuipamba nchi katika hafla mbalimbali za kitaifa, kuelimisha kizazi hadi kizazi na kuhamasisha uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Mbali na “Tanzania Yetu,” Mzee Hiza alikuwa mtunzi na mwalimu wa muziki aliyeshiriki kukuza vipaji vya vijana na kuendeleza muziki wa maadili na mafunzo.

Kazi zake zimekuwa sehemu ya urithi wa utamaduni wa taifa, zikichangia kuimarisha utambulisho wa Tanzania kupitia sanaa.

Kwa nyakati mbalimbali serikali imeonesha kutambua mchango wake katika muziki ambapo mwaka 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alimpatia zawadi ya shilingi milioni 50.