Dar es Salaam: Tanzania imeandika historia kwa kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Satelaiti ya Pamoja la SADC 2026, mkutano wa siku tano unaowakutanisha wataalamu wa anga na satelaiti kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo umeanza rasmi tarehe 16 Februari 2026 na utahitimishwa tarehe 20 Februari 2026, ukiwa ni hatua muhimu kuelekea kuifanya kanda ya SADC kuwa kinara wa teknolojia za satelaiti na uchumi wa anga barani Afrika.
Nchi za SADC zimejipanga kuanzisha Satelaiti ya Pamoja, itakayokuwa chachu ya maendeleo katika mawasiliano, usimamizi wa majanga, ufuatiliaji wa hali ya hewa, kilimo cha kisasa na upanuzi wa huduma za mtandao, hususan vijijini. Hatua hiyo inalenga kupunguza pengo la kidijitali na kuimarisha uhuru wa kiteknolojia wa ukanda.
Mkutano huo wa kimkakati katika kuimarisha uwezo wa kikanda na kuhakikisha SADC inakuwa mshindani katika uchumi wa anga wa kimataifa umewakutanisha wataalamu wa kiufundi, watunga sera na washirika wa kimataifa, wakiwemo Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) na Baraza la Umoja wa Mawasiliano Afrika (ATU), kwa lengo la kujadili maono ya sera kuwa utekelezaji wa vitendo na matokeo yanayoonekana.
Tanzania imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama na wadau wa kimataifa kuhakikisha mpango wa Satelaiti ya Pamoja unatekelezwa kwa mafanikio.
