Home ยป Tanzania yaweka rekodi kwa kuanza kutengeneza vichwa vya treni

Tanzania yaweka rekodi kwa kuanza kutengeneza vichwa vya treni

by Joshua Kiziba

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Uchukuzi na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuanza kutengeneza vichwa vya treni hapa nchini kupitia karakana ya Pugu, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza gharama za matengenezo ya treni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wenye ujuzi nchini.

Kakoso ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kupitia TRC kuendelea kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kwa kuwapatia mafunzo ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza utaalamu na ubunifu katika sekta ya reli.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema Serikali chini ya Uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi kwa kujenga miundombinu ya reli na kununua vitendea kazi vya kisasa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibwa Shiwa amesema kutengeneza vichwa vya treni katika eneo la pugu kumesaidia Watanzania wengi kupata uzoefu.

TRC iliingia mkataba na kampuni ya SMH Rail ya Malaysia mwaka 2022 kwa ajili ya uundaji wa vichwa nane vya treni za MGR Daraja la 91XX, ambapo viwili vilitengenezwa Malaysia na sita vinatengenezwa Tanzania, ambapo viwili kati ya hivyo vimekamilika.