Dar es Salaam: Rais Samia Suluhu Hassan leo amepokea ripoti muhimu inayopendekeza mabadiliko makubwa katika mfumo wa kodi nchini yanayolenga kupatia ufumbuzi malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara, na wawekezaji.
Akizungumza wakati wa kupokea taarifa hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Samia ameeleza kuwa tathmini ya mwisho ya kina kuhusu mfumo wa kodi ilifanywa takribani miaka 35 iliyopita, na hivyo tathmini hii ni muhimu kutokana na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia na kiuchumi duniani yanayolazimu kuhuisha mfumo wetu wa kodi ili kukidhi mahitaji ya sasa.
Ameahidi kufanyia kazi mapendekezo yote 284 yaliyowasilishwa na Tume kupitia mikakati ya muda mfupi, wa kati, na wa muda mrefu kwani maboresho hayo ni kiungo muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Sefue, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 18, Machi, 2026.
Serikali inalenga kujenga mfumo wa kodi wenye usawa, unaoeleweka, usio na tafsiri kinzani, na wenye kodi zisizoumiza ili kuwezesha biashara kustawi huku ikikusanya mapato. Lengo kuu la kitaifa ni kufikia uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa (Tax-to-GDP ratio) wa asilimia 18.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, ametaja baadhi ya changamoto walizobaini kuwa ni pamoja na viwango vikubwa vya kodi na tozo, udhaifu katika kutatua migogoro ya kikodi, uratibu hafifu wa taasisi zinazokusanya mapato, na wigo mdogo wa walipakodi.
Balozi Sefue ameonya juu ya mfumo wa sasa akisema, “Bila mabadiliko makubwa, Tanzania itaendelea kukusanya kodi kutoka kwa wachache, tena kwa usumbufu.”
Aidha, ameshauri Serikali kuweka mizani nzuri kati ya kukusanya kodi na kukuza uchumi kwa kusisitiza, “Hatuwezi kuvuna bila kupanda; wala kukamua maziwa bila ng’ombe kulishwa,” akimaanisha umuhimu wa kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Tathmini ya Tume inaonyesha kuwa endapo mapendekezo yote yatatekelezwa kikamilifu, Serikali inaweza kuongeza mapato yake kwa kiasi cha shilingi trilioni 11.025 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo.
