Home » Tanzania kuwa ya nne duniani uzalishaji madini ya Niobium

Tanzania kuwa ya nne duniani uzalishaji madini ya Niobium

by Joshua Kiziba

Mbeya— Tanzania imeingia hatua muhimu ya kuimarisha biashara na Marekani baada ya Serikali na Panda Hill Tanzania Limited kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Niobium wa Panda Hill, hatua inayolenga kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa madini mkakati.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi huo ni wa uzalishaji wa madini adimu ambayo hayapatikani kila mahali duniani, na kwamba Tanzania inalenga kuchukua nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa la niobium kupitia mradi huo.

Alisema soko la dunia kwa sasa linatawaliwa na wazalishaji wachache wakubwa, na Panda Hill itaiweka Tanzania kwenye ramani ya wazalishaji wakuu duniani.

Mzalishaji mkubwa duniani yupo Brazil na huzalisha takribani asilimia 80 ya mahitaji ya dunia, mzalishaji wa pili naye yupo Brazil na huzalisha takribani asilimia 11, huku Canada ikichangia takribani asilimia 6. Kupitia Panda Hill, alisema Tanzania inalenga kuwa mzalishaji wa nne duniani kwa kuchangia takribani asilimia 4 ya mahitaji ya dunia, na uzalishaji unaolengwa kufikia tani 100,000 kwa mwaka.

Niobium ni madini ya kimkakati yanayotumika kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi za utendaji wa juu zinazohitajika kwenye miundombinu, teknolojia za kisasa, magari ya umeme na injini za ndege.

Kwa mujibu wa taarifa za kampuni hiyo, mradi unahusisha ujenzi wa mgodi wa niobium pamoja na kituo cha uchenjuaji na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium, bidhaa yenye thamani iliyoongezwa inayohitajika na viwanda vya chuma na uzalishaji wa viwandani.

Panda Hill imeeleza kuwa katika maisha ya mradi, thamani ya manunuzi ya ndani inakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 1.77, huku asilimia 70 ya manunuzi ya bidhaa na huduma ikilengwa kufanyika ndani ya nchi wakati wa uzalishaji.

Kuhusu ajira, Waziri Mavunde alisema mradi unatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 1,600 kusaidia ujenzi na kutoa ajira za kudumu takriban 600, huku jumla ya watu watakaonufaika moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja ikitarajiwa kufikia takriban 7,000.

Kwa upande wa ushiriki wa Serikali, ilielezwa kuwa Tanzania itakuwa na umiliki wa hisa asilimia 16 kupitia mfumo wa free carried interest, unaolenga kuimarisha ushiriki wa Taifa katika maamuzi ya kimkakati na faida za mradi.