Home ยป Tanzania na Urusi kushirikiana kukuza sekta ya teknolojia nchini

Tanzania na Urusi kushirikiana kukuza sekta ya teknolojia nchini

by Joshua Kiziba

Tanzania imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kukua kwa sekta ya sayansi na teknolojia nchi, ili kuchochea maendeleo na kuwanufaisha wananchi hasa vijana. Katika muktadha huo, Tanzania imesaini makubaliano na Urusi ambapo utiaji saini Hati ya Makubaliano (MoU) umefanyika kati ya Taasisi ya Innopraktika kutoka nchini Urusi yenye muunganiko wa makampuni zaidi ya 142 ya Teknolojia (High Tech companies) na Kampuni ya Gen Z Corporation Limited ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania na Shirikisho la Urusi zimejizatiti kuimarisha ushirikiano katika teknolojia za kisasa, hatua inayolenga kukuza diplomasia ya uchumi kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili.

Aidha, Waziri Kombo amesema hati hiyo ya makubaliano imekuja wakati mwafaka ambapo Tanzania inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera yake Mpya ya Mambo ya Nje, inayolenga kukuza diplomasia ya uchumi, huku ikisisitiza umuhimu wa teknolojia na ubunifu kama vichocheo vya maendeleo endelevu.

Amesema teknolojia ya kisasa ni chachu muhimu katika kupunguza umaskini, kurahisisha upatikanaji wa elimu, masoko ya bidhaa, na huduma za kifedha katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo.

Sambamba na tukio hilo, waziri ameelezea kufurahishwa na pendekezo la makampuni hayo la kuanzisha โ€˜Kituo cha Teknolojia โ€“ Technology Hubโ€™ nchini Tanzania.

Amebainisha kuwa mpango huo unaendana kikamilifu na azma ya kitaifa ya kuwa kitovu cha teknolojia ya taarifa na mawasiliano (ICT) kikanda.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Innopraktikam, Alexander Likhanov amesema Hati hiyo ya Makubaliano ya ushirikiano itahusisha ushirikiano katika teknolojia za kisasa katika kuboresha ufanisi wa kazi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, mawasiliano, usafirishaji na maliasili.