Home ยป Rais Samia atunukiwa tuzo kwa mageuzi ya kimkakati sekta ya afya nchini

Rais Samia atunukiwa tuzo kwa mageuzi ya kimkakati sekta ya afya nchini

by Joshua Kiziba

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa tuzo maalum ya Ubinadamu ya Upasuaji wa Ubongo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini.

Tuzo hiyo imetolewa leo na Rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania, Dkt. Othman W. Kiloloma katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) alioufungua jijini Dar es Salaam.

“Kwa niaba ya chama cha wataalam wa upasuaji wa ubongo na mgongo tunakutambua na kukushukuru kwa mchango wako mkubwa wa ubinadamu, ni heshima yangu kubwa kukukabidhi tuzo ya ubinadamu ya upasuaji wa ubongo, hongera sana,” amesema Dkt. Kiloloma.

Amesema kuwa, kupitia uwekezaji uliowekwa na Serikali ya awamu ya sita katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, ujenzi wa rasilimali watu na uimarishaji wa huduma za vipimo, dharura na bima ya afya kwa wote umeokoa maisha na matumaini ya maisha ambayo wengine hawakuwa nayo.

Akizungumza Rais Samia amesema katika miaka mitano iliyopita kazi kubwa iliyofanyika imeleta matokeo ambapo hospitali zinazofanya upasuaji wa kibingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu zimeongezeka kutoka 2 hadi 7, madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wameongezeka kutoka 12 hadi 37, na serikali imeongeza kwa kiasi kikubwa vifaa muhimu kama MRI, CT-Scan na X-ray.

Aidha, amesema tuzo huyo ni heshima kwa Watanzania wote na ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kikanda na kimataifa kuimarisha huduma za afya kwa kuzifanya kuwa bora, nafuu na za uhakika ili kuokoa maisha ya wananchi na kurejesha tumaini kwa jamii.