Home ยป Bugando yaandika historia kwa kufanya upandikizaji wa figo kwa mara ya kwanza

Bugando yaandika historia kwa kufanya upandikizaji wa figo kwa mara ya kwanza

by Joshua Kiziba

Mwanza: Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando imefanikiwa kufanya upasuaji wa upandikizaji figo, hatua inayofungua ukurasa mpya wa huduma za kibingwa bobezi kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Upasuaji huo wa mafanikio umefanyika kwa mgonjwa mwenye umri wa miaka 40 (mwanaume), mkazi wa Mkoa wa Mwanza, kwa ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu wa Hospitali ya Bugando na timu ya wataalamu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Sr. Dkt Alicia Massenga, amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa sekta ya afya nchini, na serikali kwa ujumla.

“Leo Bugando imeandika historia, kuanzishwa kwa huduma hii ya upandikizaji figo ni mkombozi kwa maelfu ya wananchi wa kanda hii, maandalizi yalikua ya muda mrefu lakini leo hii tumefanikiwa kufanikisha zoezi hili,” amesema.

Sr. Massenga ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji kwa ushirikiano wa Baraza la Maaskofu (TEC) na Serikali katika miundombinu, vifaa, na mafunzo kwa wataalamu.

“Huu ni uthibitisho kuwa ushirikiano baina ya hospitali hizi unaokoa maisha ya Watanzania. Tunakusudia kufanya upandikizaji kwa wagonjwa wengine hapa Bugando kuanzia sasa, tunawakaribisha sana kwa huduma hii,” ameongeza.

Kwa upande wake kiongozi wa timu kutoka Benjamini Mkapa, Prof. Masumbuko Mwashambwa,ย  Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka UDOM na pia kiongozi wa timu ya upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma akiiwakilisha Timu hii ya wataalamu amesema, wapo tayari kuendelea kushirikiana na Bugando wakati wote.