Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kugharamia maadhimisho ya Sherehe za Muungano mwaka huu, zitumike kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchembaleo ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma alipokuwa akiuarifu umma kuhusu maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano wa Tanzania yatakavyofanyika.
“Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Muungano yatafanyika katika ngazi ya mikoa yote nchini ambapo viongozi wakuu wa kitaifa watafanya shughuli za kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, amesema imeelekezwa kuwa wakuu wa mikoa watembelee, waweke mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kushiriki shughuli za usafi wa mazingira, kupanda miti na kufanya mashindano ya michezo mbalimbali.
Shughuli nyingine zitakazoambatana na maadhimisho hayo ni mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali, mashindano ya uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari, mahojiano maalum na wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi sasa.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni: “MIAKA 62 YA MUUNGANO: AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO NI MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU.”
