Home ยป Tanzania na Kenya zatia saini mikataba nane, zakubaliana kumaliza vikwazo vya biashara

Tanzania na Kenya zatia saini mikataba nane, zakubaliana kumaliza vikwazo vya biashara

by Joshua Kiziba

Tanzania na Kenya zimekubaliana kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili, wakidhamiria kumaliza vikwazo vilivyosalia ifikapo mwisho wa Mei, 2026.

Aidha, zimekubaliana kuimarisha Kamati za Pamoja za Biashara zitakazokutana mara kwa mara kushughulikia changamoto zilizopo na kuzuia kuibuka kwa vikwazo vipya vinavyoweza kuathiri biashara baina ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania, na Rais wa Kenya, William Ruto ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili.

Katika hatua nyingine, viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba na hati nane za makubaliano katika maeneo ya reli, upembuzi yakinifu wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, usaidizi wa kisheria katika makosa ya jinai, kilimo, utambuzi wa vyeti vya mabaharia, usimamizi wa usafiri wa majini, viwango kati ya Zanzibar na Kenya, pamoja na kujengeana uwezo katika utumishi wa umma.

Vilevile, Rais Dkt. Samia na Rais Ruto wameshiriki Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Kenya, lililowakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji na sekta binafsi kutoka nchi zote mbili.

Katika kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya wamewasilisha uzoefu wa uwekezaji wa pande mbili na kueleza haja ya kuongeza ushirikiano katika viwanda, nishati, fedha, kilimo, miundombinu na huduma.