WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji amesema matokeo ya Sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori Wakubwa, wa Kati na Wadogo yameonesha mwenendo chanya wa uhifadhi, huku idadi yao ikiongezeka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Dkt. Kijaji amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori iliyofanyika mapema leo jijini Arusha
“ Matokeo ya Sensa hii yanaonesha Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza Afrika kwa utajiri wa rasilimali za wanyamapori,” amefafanua Dkt.Kijaji.
Matokeo hayo yaliyotangazwa leo Juni 17, 2026 jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanaonesha pia uwepo wa aina 28 za wanyamapori wa ukubwa wa kati na wakubwa katika mifumo yote ya ikolojia iliyohesabiwa nchini.
Sensa hiyo ya Mwaka 2024/2025 imefanyika miaka 10 baada ya ile ya Mwaka 2014 na imehusisha maeneo yote yenye wanyamapori, yakiwemo maeneo yaliyohifadhiwa, maeneo ya mtawanyiko, shoroba za wanyamapori na maeneo mengine muhimu ya ikolojia.
Akizungumza katika tukio hilo Dkt. Kijaji alisema sensa imebaini mafanikio makubwa ya juhudi za uhifadhi zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
“Matokeo yanaonesha kuwa idadi na mwenendo wa wanyamapori nchini umeendelea kuwa chanya. Hii ni ishara kuwa hatua zinazochukuliwa katika uhifadhi wa rasilimali hizi zinaendelea kuzaa matunda,” alisema.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya jamii mahususi za wanyamapori zilizofanyiwa tathmini, aina saba zimeonesha ongezeko la idadi ya wanyamapori, aina 11 zimeendelea kuwa katika hali ya kuimarika huku aina moja pekee ikionesha kupungua na hivyo kuhitaji hatua za haraka za uhifadhi ili kuzuia hatari ya kutoweka.
Aidha, sensa imeendelea kuthibitisha nafasi ya Tanzania kama moja ya nchi tajiri kwa wanyamapori barani Afrika. Tanzania inaongoza Afrika kwa idadi ya nyati 328,437 na simba 17,200.
Pia Tanzania ipo katika nafasi ya tatu kwa idadi ya tembo wanaokadiriwa kufikia 66,700 na nafasi ya nne kwa idadi ya faru weusi na weupe 302.
