Home HabariTanzania, Misri Zakubaliana Kupanua Ushirikiano wa Kimkakati

Tanzania, Misri Zakubaliana Kupanua Ushirikiano wa Kimkakati

by Joshua Kiziba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, wamekubaliana kupanua ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na viwanda.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi, Rais Samia amesema viongozi hao wameelekeza taasisi za pande zote mbili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi pamoja na kutumia kikamilifu fursa za Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Akizungumzia kuhusu sekta ya miundombinu na uchukuzi, Rais Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa wamejadili na kukubaliana kuhusu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na reli ya kuunganisha Bagamoyo na Bandari Kavu ya Kwala. Vilevile, wamekubaliana kuendelea kuimarisha usafiri wa anga, huku Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) likijiandaa kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Misri, pamoja na kuendeleza ushirikiano kati ya ATCL na EgyptAir.

Naye Mheshimiwa Rais El-Sisi ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Misri ni wa kimkakati na wa kudumu. Amesisitiza kuwa dhamira ya Misri ni kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili.

Vilevile, Rais Mheshimiwa El-Sisi imeeleza utayari wake wa kushirikiana na Tanzania katika katika sekta ya afya, ikiwemo kujenga hospitali pamoja na kuimarisha huduma za kibingwa na mafunzo kwa wataalam wa afya.

Rais El-Sisi ameongeza kuwa Misri inatarajia kuongeza biashara na ushirikiano na Tanzania katika kilimo, vifaa tiba na sekta nyingine za kimkakati. Pia amepongeza kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere na kueleza matumaini kuwa ushirikiano huo utaendelea kukua kwa manufaa ya nchi na wananchi wa pande zote mbili.

Tanzania na Misri zitashirikiana katika Ranchi ya Taifa ya Ruvu pamoja na kukuza ushirikiano pamoja na kushirikiana na Taasisi za Tanzania, ikiwemo JKT, Magereza na NARCO ambazo zina maeneo makubwa yenye kufaa kwa kilimo na ufugaji.