Home HabariSerikali yatenga bilioni 300 kupanua mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi

Serikali yatenga bilioni 300 kupanua mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi

by Joshua Kiziba

DODOMA: Serikali imeongeza uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kupanua upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza tija katika minyororo ya thamani ya sekta hizo.

Hatua hiyo imetangazwa leo katika kilele cha Maonesho na Sherehe za Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) mkoani Dodoma, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh300 bilioni kwa benki saba zitakazotekeleza mpango huo.

Benki hizo ni CRDB, Stanbic, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Tanzania Commercial Bank (TCB), Azania Bank, Benki ya Ushirika na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza rasilimali katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, sambamba na kuongeza bajeti za kisekta na kuimarisha mtaji wa TADB ili kuiwezesha kutoa mikopo kwa shughuli za kilimo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema Serikali imeongeza mtaji wa TADB kwa ajili ya shughuli za kilimo, akisisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuonekana kupitia ongezeko la tija, uzalishaji, masoko na kipato cha wananchi.

“Tunataka kuona ufanisi huu ukitoa matokeo ya moja kwa moja; tuone mkulima, mvuvi na mfugaji ananufaika kule alipo na anaongeza kipato chake,” amesema Rais Samia.

Amesema Serikali itaendelea kutafuta masoko ya ndani na nje, huku ikipanua ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji, uwekezaji na kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi.

Rais Samia pia ameiagiza Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA) kuimarisha utoaji wa huduma kwa wazalishaji na kukamilisha mifumo ya kidijitali ya kusimamia huduma za ugani nchini.

Amesisitiza pia umuhimu wa uzalishaji kuongozwa na taarifa za soko, akitaja tumbaku, kahawa na mazao ya baharini kuwa miongoni mwa bidhaa ambazo uzalishaji wake umechochewa na upatikanaji wa taarifa za masoko ya dunia.

Vituo vya biashara vya mahindi na mpunga

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema Serikali imeanza maandalizi ya vituo vya kimkakati vya biashara ya mahindi na mpunga katika maeneo manne nchini.

Amesema vituo hivyo vitasaidia kuimarisha masoko na uhifadhi wa mazao, pamoja na kupunguza upotevu unaotokea baada ya mavuno.

Chongolo pia amesema Serikali imefikia makubaliano ya kibiashara na Jamhuri ya Sudan Kusini yatakayowezesha mazao ya kilimo kutoka Tanzania kuuzwa moja kwa moja nchini humo.

Amesema hatua hiyo imefuatia ushiriki wa ujumbe wa Sudan Kusini katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu, huku wafanyabiashara zaidi kutoka nchini humo wakitarajiwa kushiriki katika maonesho hayo mwaka 2027.

Sh30 bilioni zimetolewa kwa mifugo na uvuvi

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema wizara yake tayari imepokea Sh30 bilioni kati ya Sh200 bilioni zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na makundi maalum.

Amesema Sh7 bilioni tayari zimetolewa kwa walengwa, huku Sh23 bilioni zikitarajiwa kutolewa kupitia TADB kwa ajili ya shughuli za mifugo na uvuvi.

Sekta binafsi yasifu ushirikiano na Serikali

Akizungumza kwa niaba ya sekta binafsi, Rais wa Shirikisho la Wakulima Tanzania, Jitu Vrajlal Son, amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi utaongeza ufanisi katika kupanga vipaumbele vya kilimo na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema ushirikiano huo unaweza pia kuharakisha uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea nchini kwa kutumia malighafi zinazopatikana Tanzania, ikiwemo gesi asilia.

Mwenyekiti wa Wabia wa Maendeleo katika Kilimo, Dkt. Nyabenyi Tito Tipo, amesema Maonesho ya Nanenane yameonyesha uwezo wa Tanzania kujenga sekta ya kilimo yenye tija, ushindani na ustahimilivu kupitia uwekezaji, sera wezeshi na ushirikiano.

Amesema Wabia wa Maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali kuimarisha uwekezaji katika minyororo ya thamani, teknolojia za kidijitali, kilimo himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa fedha na masoko.