Home HabariBoT yanunua tani 28 za dhahabu zenye thamani ya trilioni 9.7

BoT yanunua tani 28 za dhahabu zenye thamani ya trilioni 9.7

by Joshua Kiziba

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kwamba katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, Benki Kuu ya Tanzania imenunua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu, zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68 (thamani ya dhahabu iliyopo kwa bei ya jana), sawa na shilingi trilioni 9.76, ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, thamani ya shilingi, uthabiti wa sekta ya fedha na ukuaji wa uchumi.

Bw. Tutuba aliyasema hayo wakati akishiriki mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu ya Benki Kuu (Central Bank Gold Operations), ikiwa ni sehemu ya mijadala ya Mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), African Caucus 2026, unaozihusisha nchi 54 za Afrika, unaofanyika Banjul nchini Gambia.

Alisema kuwa mpango huo wa kununua dhahabu si tu kwamba umeiwezesha nchi kuhifadhi dhahabu kama mbadala wa kutunza fedha za kigeni, lakini pia umeongeza urasimishaji kwenye sekta ya madini na ujumuishi wa kifedha kwa wauza madini hayo, wakiwemo wachimbaji wadogo, ambapo Benki Kuu imewezesha makundi hayo kufungua zaidi ya akaunti 4,000 katika taasisi mbalimbali za fedha hususan benki.

Gavana Tutuba alieleza kuwa kutokana na bei nzuri ya soko ambayo Benki Kuu inatoa kwa wafanyabiashara wa madini, kumekuwa na mwitikio chanya wa wafanyabuashara na wachimbaji kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania.

“Tunawalipa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kwa wakati, ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa mauzo, na tunawalipa kwa bei ya soko la dhahabu la London ya siku hiyo, hatua inayowavutia kuiuzia dhahabu Benki Kuu.” Alisema Gavana Tutuba.