Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Aprili 11, 2026, ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima na Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa, Keffi nchini Nigeria. Hafla hiyo imefanyika kwa njia ya mtandao huku Rais akifuatilia akiwa Ikulu, Dodoma.
Chuo hicho kimempa heshima hiyo kutambua mchango wake mkubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuimarisha afya ya mama na mtoto, kuendeleza uongozi wa wanawake barani Afrika pamoja na kusimamia ajenda za biashara, hususan kwa vijana.
Tija kwa Tanzania
Kutunukiwa kwa heshima hii kuna manufaa makubwa kwa Tanzania kimataifa na kitaifa. Kwanza, kunaiweka Tanzania katika ramani ya nchi zinazoongoza katika ajenda za maendeleo endelevu, hasa katika sekta ya nishati safi na afya ya jamii. Pili, kunaimarisha diplomasia ya kimataifa kwa kuongeza ushawishi wa Tanzania katika Afrika na duniani, jambo linaloweza kuvutia uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati.
Aidha, heshima hiyo inaongeza hadhi ya nchi katika kukuza usawa wa kijinsia na uongozi wa wanawake, ikiwa ni mfano chanya kwa mataifa mengine. Pia, inawapa motisha vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na ubunifu, wakitambua kuwa juhudi zao zinaweza kutambulika kimataifa.
Shahada nyingine za Heshima
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutunukiwa shahada za heshima. Awali, ametunukiwa shahada mbalimbali kutoka vyuo vikuu tofauti duniani.
Shahada ya kwanza ya heshima ya udaktari, alitunukiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Novemba 30, mwaka 2022.
Hiyo ilifuatiwa na shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, Oktoba 10, 2023.
Tunu ya shahada hizo haikuishia hapo, mkuu huyo wa nchi alitunukiwa shahada nyinyine ya heshima ya udaktari ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Desemba 28, 2023.
Kama hiyo haitoshi Aprili 18, 2024, Rais Samia ametunukiwa shahada nyingine ya heshima na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki.
Kwa ujumla, tuzo hizi zinaakisi namna ambavyo uongozi wa Rais Samia unavyotambulika kimataifa na kuthaminiwa kama mfano wa mageuzi chanya barani Afrika.
Hitimisho
Kutunukiwa kwa Shahada hii ya Uzamivu ya Heshima ni uthibitisho wa nafasi ya Tanzania kama taifa linalochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ni heshima si kwa Rais pekee, bali kwa Watanzania wote, na inaendelea kuimarisha taswira ya nchi katika jukwaa la kimataifa.
