Dar es Salaam. Wizara ya Maendeleo ya Vijana imeanika wazi mwongozo kwa vijana namna ya kuomba na kunufaika na mikopo ya Sh200 bilioni ambayo imekuwa ikitangazwa na Serikali kuwa lengo lake ni kuwawezesha kiuchumi.
Katika mwongozo huo, serikali imeeleza kuwa waombaji ni mtu mmoja au kikundi na wanatakiwa kuwa na andiko la mradi au biashara, akaunti ya benki au namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mwombaji au kikundi hicho, pamoja na kuwasilisha barua rasmi ya maombi ikieleza aina ya mradi, kiasi cha mkopo na eneo la utekelezaji.
Aidha, nyaraka muhimu zimetajwa kuwa ni pamoja na kitambulisho cha Taifa (NIDA) au cha mpiga kura, TIN, leseni ya biashara kwa wanaoendesha shughuli tayari, barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa na picha mbili za mwombaji, huku maombi yote yakitakiwa kuwasilishwa kabla ya Aprili 3, 2026 kupitia barua pepe maalum ya mikopo@vijana.go.tz
Hatua hiyo imejibu malalamiko na mapendekezo ya vijana ambao kwa nyakati tofauti tangu kutolewa kwa taarifa ya fedha hizo wamekuwa wakijitokeza wakisema hakuna uwazi wa utaratibu wa upatikanaji wake na kushauri kuwepo kwa mfumo unaoeleweka na unaowafikia wote.
Vikundi mbalimbali vya vijana vikiwemo vya vyama vya siasa, wanaharakati na makundi ya kibiashara vimekuwa vikieleza sintofahamu yao kuhusu mgawanyo wa fedha hizo, vigezo vya utoaji na taasisi husika za usimamizi, huku baadhi yao wadai kuwa taarifa zinazotolewa hazijakamilika.
Licha ya lengo la fedha hizo kuwa ni kupunguza changamoto za ajira, mitaji na kukuza uchumi wa vijana, mjadala umeendelea kutawala juu ya namna bora ya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa kwa haki na kwa ufanisi, jambo lililopelekea shinikizo la kutaka mwongozo rasmi wa kitaifa.
