Watanzania wanatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa na ujenzi wa matanki 15 ya kupokea na kusambaza mafuta katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam. Sehemu ya manufaa hayo inatarajiwa kuwa utulivu wa bei ya mafuta, na uhakika wa upatikanaji wake, hasa kunapokuwa na changamoto katika soko la duniani.
Mradi huu unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 701.8, ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 41, ukitarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2027.
Takwimu za mradi:
Ukubwa na Uwezo: Mradi unajumuisha ujenzi wa matanki 15 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya mita za ujazo 378,000 za mafuta. Hii inajumuisha mita za ujazo 162,000 za dizeli, 135,000 za petroli, na 81,000 za mafuta ya ndege (Jet A1).
Ongezeko la Uhifadhi: Kukamilika kwa mradi huu kutaongeza uwezo wa bandari wa kupokea mafuta kwa asilimia 35.9, kutoka mita za ujazo milioni 1.05 zilizopo sasa hadi kufikia mita za ujazo 1.42.
Uokoaji wa Muda: Muda wa meli kusubiri kuingia gati tangu inapofika bandarini utapungua kutoka wastani wa siku 22 hadi siku 7, na muda wa kuhudumiwa inapoingia gatini utapungua kutoka siku 7 hadi saa 24.
Manufaa kwa Taifa: Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuiweka Tanzania kama kitovu cha biashara cha kikanda. Kwa kupunguza muda wa meli kusubiri kushusha mzigo, Taifa litaokoa gharama za ucheleweshaji (demurrage) zinazofikia Dola za Marekani 25,000 (sawa na shilingi milioni 58) kwa siku kwa meli.
Ufanisi huu utavutia meli nyingi zaidi kutumia Bandari ya Dar es Salaam, hivyo kuimarisha mapato ya Taifa.
Zaidi ya hayo, mradi utaimarisha Akiba ya Kimkakati ya Hifadhi ya Mafuta ya Taifa ili kulinda nchi dhidi ya misukosuko ya soko la dunia, huku ukiunganishwa na mfumo mpya wa usafirishaji kwa njia ya reli ya kisasa (SGR) kwenda Dodoma na bandari kavu za Morogoro, Dodoma, na Shinyanga ili kupunguza msongamano bandarini.
Manufaa kwa Mwananchi:
Utulivu na Unaafuu wa Bei ya Mafuta: Kuondolewa kwa tozo za ucheleweshaji wa meli (Shilingi milioni 58) ambazo awali zilikuwa zikijumuishwa katika gharama za uagizaji na kuathiri bei ya mwisho, kutasaidia kushusha au kutuliza bei ya mafuta kwa mtumiaji wa mwisho kwenye vituo vya mafuta.
Uhakika wa Upatikanaji wa Nishati: Mwananchi hataathiriwa tena na uhaba wa mafuta mara kwa mara. Kuongezeka kwa uwezo wa kuhifadhi mafuta kunahakikisha kuwa nishati itakuwepo muda wote, jambo ambalo litawezesha sekta za uzalishaji (kama kilimo, usafirishaji, na viwanda vidogo) kufanya kazi bila usumbufu, na hivyo kurahisisha maisha ya wananchi.
