Home ยป Mradi wa umeme Kishapu wakamilika, Megawati 50 kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa

Mradi wa umeme Kishapu wakamilika, Megawati 50 kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa

by Joshua Kiziba

Shinyanga: Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua Kishapu mkoani Shinyanga uliogharimu shilingi bilioni 118.6 umekamilika, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika kwa Watanzania.

Machi Mosi mwaka huu megawati 50 zitakuwa zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likiwa katika hatua za mwisho kupata mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo itakayozalisha megawati 100 kwa gharama ya shilingi bilioni 200.4.

Tanzania inalenga kufikia uzalishaji umeme megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, ambapo kwa mujibu wa TANESCO hadi Februari 2026 uwezo wa mitambo ya kufua umeme kwenye Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya megawati 3,975.5 wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme yalikuwa megawati 2,071.3.

Hata hivyo, katika bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2025/26, serikali ilieleza kuwa uzalishaji umeme umeongezeka na kufikia megawati 4,031.71 Aprili mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 86.6 ikilinganishwa na megawati 2,138 zilizokuwepo Machi 10, 2024.

Mradi wa umeme wa jua Kishapu ni alama ya mabadiliko na hatua muhimu katika mwelekeo wa Tanzania kutumia nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme.