Home » PPAA yazuia zabuni za bilioni 586 kwa wazabuni wasio na sifa

PPAA yazuia zabuni za bilioni 586 kwa wazabuni wasio na sifa

by Joshua Kiziba

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeeleza kuwa katika uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kuzuia utoaji wa tuzo za zabuni 43 zenye thamani ya shilingi bilioni 586.5 kwa wazabuni waliokosa uwezo wa kifedha na sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika.

Aidha, imetoa fursa kwa vijana 878 kwa kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuwasilisha malalamiko na rufaa katika mfumo wa (NeST) ili kuwawezesha kudai haki kwa ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma.

Mafunzo hayo yametolewa katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuwawezesha vijana na makundi maalum kushiriki kikamilifu katika sekta ya ununuzi wa umma.

Pia, mamlaka hiyo imekamilisha ujenzi wa Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya ununuzi wa umma ambayo ni njia rahisi, ya haraka na yenye uwazi kwa wadau wote kushiriki katika mchakato wa usulushi wa migogoro ya ununuzi.