Home ยป Rais Samia aridhia watumishi 219,042 kupandishwa madaraja

Rais Samia aridhia watumishi 219,042 kupandishwa madaraja

by Joshua Kiziba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ridhiwani Kikwete, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kupandishwa madaraja watumishi wa umma 219,042 nchini, hatua inayolenga kuimarisha motisha na ufanisi katika utumishi wa umma.

Amesema hayo Mei 6, 2026 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Pili wa mwaka wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma (AAPAM), Tanzania.

Ridhiwani amewataka maafisa rasilimali watu kuhakikisha wanawasilisha taarifa kwa wakati pale wanapokutana na changamoto katika mchakato wa kupandisha madaraja ili kuepuka ucheleweshaji usio wa lazima.

Amesisitiza umuhimu wa kutenda haki kwa watumishi ili kufanikisha dhamira ya Rais ya kuboresha utendaji na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, amewataka kushughulikia kwa wakati changamoto za barua za uhamisho pamoja na kufuata taratibu rasmi kabla ya kumwondoa mtumishi kazini.

Pia amesisitiza umuhimu wa utoaji wa ushauri nasaha kwa watumishi ili kulinda afya ya akili na kuongeza tija katika utendaji wa kazi.