DAR ES SALAAM – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwelekeo mpya kwa kuitaka kuimarisha ukusanyaji wa kodi kwa misingi ya haki, weledi na huduma bora kwa walipakodi ili kuendelea kujenga Taifa linalojitegemea.
Akizungumza Julai 1, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Miaka 30 ya TRA na hafla ya utoaji wa Tuzo ya Rais kwa Walipakodi Bora, Rais Dkt. Samia amesema kodi si adhabu kwa wafanyabiashara wala mzigo kwa wananchi, bali ni mchango muhimu unaowezesha Serikali kuboresha huduma za jamii, kuendeleza miundombinu na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Maelekezo kwa TRA
Rais Dkt. Samia ameitaka TRA kupunguza kero kwa walipakodi, kurahisisha utoaji wa huduma na kuongeza elimu ya kodi kwa wananchi. Pia amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kupunguza muda wa huduma, gharama na migogoro, huku akielekeza maboresho hayo yakamilike kabla ya mwisho wa kipindi chake cha uongozi.
Aidha, amesema mapambano dhidi ya ukwepaji kodi, magendo na mianya ya upotevu wa mapato yanapaswa kwenda sambamba na utoaji wa huduma rafiki kwa walipakodi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara. Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti rushwa na kuendelea kujenga imani kati ya TRA na wananchi.
Makusanyo ya Kodi Yaendelea Kuongezeka
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema makusanyo ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 532 mwaka wa fedha 1996/1997 hadi zaidi ya shilingi trilioni 37.957 mwaka wa fedha 2025/2026.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ukuaji wa uchumi, kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari, maboresho ya mifumo ya ukusanyaji na usimamizi madhubuti wa mapato. Pia amesema uwezo wa TRA kutoa huduma umeongezeka, ambapo idadi ya watumishi imefikia zaidi ya 8,000 kutoka chini ya 500 wakati mamlaka hiyo ilipoanzishwa.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza TRA kwa mafanikio yake na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na mamlaka hiyo katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuongeza ufanisi wa huduma.
Walipakodi Bora Watunukiwa
Katika kilele cha maadhimisho hayo, Rais Dkt. Samia alikabidhi tuzo 54 kwa walipakodi bora kutoka makundi mbalimbali, ikiwa ni kutambua mchango wao wa kulipa kodi kwa uaminifu, kwa wakati na kwa kuzingatia sheria.
Aidha, aliwatunuku Makamishna Wakuu wastaafu wa TRA kwa kutambua mchango wao katika kujenga na kuimarisha taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Kwa upande wake, TRA ilimtunuku Rais Dkt. Samia Tuzo Maalum ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari na kuendeleza ajenda ya Taifa ya kujitegemea.
