Home ยป Rais Samia kupunguza msafara wake ili kubana matumizi ya mafuta serikalini

Rais Samia kupunguza msafara wake ili kubana matumizi ya mafuta serikalini

by Joshua Kiziba

Dodoma: Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amechukua hatua madhubuti za kubana matumizi ya mafuta serikalini kwa kuelekeza kuwa watumishi na maafisa wa ofisi yake watakaofuatana naye katika safari za kikazi watatumia usafiri wa pamoja.

Rais Samia amebainisha kuwa kuanzia sasa, watendaji hao watatumia mabasi ili kupunguza idadi ya magari, gharama za uendeshaji, na matumizi ya mafuta katika kipindi hiki ambacho bei ya mafuta imepanda duniani.

Aidha, amezitaka wizara na taasisi nyingine zote za serikali kuchukua hatua kama hizo za makusudi ili kupunguza matumizi ya mafuta.

Ameeleza kuwa uamuzi huo umechangiwa na hali ya vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, ambavyo vimeathiri nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania, kwa kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa nyingine.

Pamoja na changamoto hizo za kidunia, Rais amebainisha kuwa Tanzania bado ipo katika hali nafuu ya upatikanaji wa mafuta ikilinganishwa na nchi nyingine.

Rais Samia amewatahadharisha wafanyabiashara nchini kutotumia kupanda kwa bei ya mafuta kama kisingizio cha kupandisha bei za bidhaa kiholela. Amesisitiza kuwa ni kosa kufanya hivyo, hususan kwa bidhaa ambazo tayari zipo maghalani na hazikuathiriwa na mabadiliko ya sasa ya bei.