Home HabariRais Samia kuzindua meli za mizigo Ziwa Victoria

Rais Samia kuzindua meli za mizigo Ziwa Victoria

by Joshua Kiziba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anatarajiwa kuzindua meli nne mpya za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 2,000 kila moja mkoani Kigoma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema meli hizo zimetengenezwa na kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited kutoka China na zitawezesha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia kupitia njia ya majini.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuifanya Kigoma kuwa lango muhimu la biashara kuelekea Afrika ya Kati kwa kuimarisha usafiri fungamanishi unaounganisha reli, bandari na usafiri wa majini. Takwimu zinaonesha Bandari za Ziwa Tanganyika zilihudumia tani 815,285 za shehena mwaka wa fedha 2025/26, ongezeko kutoka tani 397,897 mwaka 2024/25.

Serikali pia imepanga kuboresha Bandari ya Kigoma kwa kujenga gati la kisasa la abiria na mizigo ili kuongeza uwezo wa kuhudumia meli mpya na zilizopo. Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za biashara, uwekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika ukanda wa Maziwa Makuu.