Kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abdel Fattah El-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, atafanya Ziara ya Kitaifa nchini tarehe 18 Julai, 2026.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam na baadaye kuwa na mazungumzo ya pande mbili na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pamoja na mambo mengine muhimu, mazungumzo ya viongozi hao yanatarajiwa kujikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, katika sekta za kiuchumi, sambamba na kutafuta fursa mpya za ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kati ya nchi hizi mbili. Ziara hiyo pia itatoa fursa ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri.
Aidha, Waheshimiwa Marais hao watazungumza kwa pamoja na waandishi wa habari, kuelezea yaliyojiri kwenye mazungumzo yao na kuhusu dhamira yao ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Misri.
Vilevile, Viongozi hao watazindua Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Misri, litakalowakutanisha wawekezaji, wafanyabiashara, wawakilishi wa sekta binafsi na viongozi waandamizi wa Serikali kutoka nchi hizo mbili. Jukwaa hilo litatoa fursa ya kujadili na kuibua maeneo mapya ya uwekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, pamoja na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa lengo la kuleta ustawi wa pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wa nchi hizo mbili.
Ziara ya Mheshimiwa Rais Abdel Fattah El-Sisi ni kielelezo kingine cha uhusiano imara wa kihistoria na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri. Aidha, ziara hiyo inatarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo, na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati.
