Rais wa Jamhuri ya Singapore, Tharman Shanmugaratnam, atafanya ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia tarehe 8 hadi 10 Juni 2026, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hii ni ziara ya kwanza ya kiserikali ya Rais wa Singapore nchini Tanzania tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili tarehe 12 Desemba 1980, na inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Singapore.
Ziara hiyo inalenga kuendeleza ubia wa kimkakati na kukuza maendeleo ya kiuchumi kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, maendeleo ya bandari na usafirishaji, uchumi wa kidijitali, utalii, elimu, mafunzo na ukuzaji wa ujuzi, pamoja na miundombinu na teknolojia.
Rais Tharman, akiambatana na mkewe, Jane Ittogi Shanmugaratnam, mawaziri, maafisa waandamizi wa Serikali na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Singapore, atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 8 Juni 2026. Atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabiti Kombo.
Tarehe 9 Juni 2026, Rais Tharman atapokelewa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Viongozi hao watafanya mazungumzo ya faragha na baadaye mazungumzo rasmi yatakayojikita katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili. Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watatoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari.
Siku hiyo hiyo, Rais Samia na Rais Tharman watashiriki Jukwaa la Biashara na Uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Singapore kwa lengo la kuchochea fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi. Baadaye, Rais Tharman atahudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake.
Mnamo tarehe 10 Juni 2026, Rais Tharman atafanya ziara Zanzibar ambako atakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Baadaye jioni, yeye na ujumbe wake wataondoka kurejea Singapore.
Ziara hii ya kihistoria inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore, hususan katika maeneo ya uwekezaji, biashara, maendeleo ya miundombinu, ubunifu wa teknolojia na kubadilishana uzoefu wa maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
