Rais wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, yupo nchini Tanzania kwa ziara ya kitaifa.
Ziara hiyo ya kihistoria inaakisi uhusiano wa karibu, wa muda mrefu na wa kindugu kati ya Tanzania na Namibia, na inatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Historia ya uhusiano kati ya Tanzania na Namibia
Tanzania na Namibia zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia katika ngazi ya nchi mbili (bilateral), kikanda na kimataifa. Uhusiano huo umejengwa juu ya msingi imara wa kihistoria unaotokana na kipindi cha mapambano ya uhuru, ambapo waasisi wake, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Samuel Nujoma, walishirikiana katika harakati hizo, jambo lililoweka msingi imara wa urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Leo hii, uhusiano huo unaendelea kuimarishwa kupitia ziara za viongozi wakuu, mikataba ya ushirikiano na majukwaa ya kikanda kama Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika
Mauzo ya Tanzania na Namibia
Mauzo makuu ya Tanzania kwenda Namibia ni pamoja na: mashine za frontend shovel loaders, stempu za posta, mihuri ya posta, vifaa vya posta na vinavyofanana na hivyo, pamoja na vipuri na vifaa vya ziada, na chanjo za tiba ya mifugo.
Kwa upande mwingine, bidhaa kuu zinazoagizwa kutoka Namibia ni pamoja na: bia, mvinyo wa gesi (sparkling wine), wiski, pamba, cider, liqueurs na cordials.
Ushirikiano wa kiuchumi
Licha ya uhusiano mzuri wa kihistoria, mataifa haya mawili bado hayajanufaika kikamilifu na ushirikiano wa kiuchumi. Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo ni kidogo, ambapo mwaka 2024 kilikuwa shilingi bilioni 20, kikipungua kutoka shilingi bilioni 20.3 mwaka 2023.
Ingawa uhusiano wa kisiasa ni imara, biashara kati ya nchi hizo bado haijakua kwa kiwango kikubwa. Takwimu zinaonesha kuwa biashara kati ya Tanzania na Namibia imekuwa chini ya shilingi bilioni 21 kwa mwaka.
Hata hivyo, kuna fursa katika sekta mbalimbali ambazo hazijatumika kikamilifu. Namibia inaendelea kukua katika sekta ya mafuta na gesi, ikiwa na akiba kubwa ya mafuta katika Bonde la Orange na gesi ya asili, jambo linaloweza kuiweka Namibia miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani ifikapo 2035. Pia ina gesi ya takriban futi trilioni 8.7 za ujazo.
Kwa upande wa Tanzania, ina akiba kubwa ya gesi barani Afrika inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57.5. Hii ni fursa ya nchi hizo mbili kushirikiana kupitia kubadilishana uzoefu na kuimarisha taasisi za mafuta na gesi.
Uwekezaji
Kuanzia mwaka 1997 hadi Desemba 2024, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi mitatu pekee kutoka Namibia. Miradi hiyo ina thamani ya takriban dola za Marekani milioni 6.98 na imezalisha ajira 21. Miradi hiyo imesajiliwa katika sekta za utalii na mawasiliano ya simu.
Madini
Tanzania na Namibia zina utajiri wa madini mbalimbali kama almasi, dhahabu, shaba, chuma na madini adimu. Hii inatoa nafasi ya kushirikiana katika kubadilishana uzoefu na ujuzi kwa manufaa ya uchumi wa pande zote.
Kilimo na Mifugo
Namibia inakabiliwa na ukame na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri uzalishaji wa chakula, na hivyo huagiza asilimia 60 hadi asilimia 80 ya chakula chake. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha chakula kwa wingi barani Afrika, hivyo ina nafasi ya kuuza bidhaa kama mchele na mahindi kwenda Namibia.
Kwa upande mwingine, Namibia imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na mifugo. Nchi hiyo ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa nyama ya ng’ombe barani Afrika na pia ina maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa samaki duniani.
Utalii, usafiri na utamaduni
Tanzania na Namibia pia ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii barani Afrika. Ushirikiano katika sekta ya utalii unatarajiwa kuimarika kupitia matangazo ya pamoja na kuanzisha miundombinu ya usafiri kama safari za moja kwa moja za ndege kati ya nchi hizo mbili.
Katika upande wa utamaduni, Kiswahili kimeendelea kuwa daraja muhimu la mshikamano. Tanzania imekuwa ikihamasisha ufundishaji wa Kiswahili nchini Namibia, na juhudi za ushirikiano katika elimu zinaendelea.
Afya na Elimu
Mfumo wa afya wa Namibia unaendelea kuimarika, lakini unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma na uhaba wa wataalamu. Tanzania kwa upande wake imepiga hatua katika huduma za kibingwa kama magonjwa ya moyo, saratani na figo pamoja na mafunzo ya wataalamu wa afya.
Hii inatoa fursa ya ushirikiano kupitia mafunzo ya pamoja, ubadilishanaji wa wataalamu, na misheni za matibabu. Pia Tanzania imewahi kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Namibia katika taasisi kama Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kilimanjaro Christian Medical Centre na Hubert Kairuki Memorial University.
Viongozi wanawake na sura mpya ya ushirikiano
Uhusiano huu pia unaingia hatua mpya ya kihistoria kwa kuwa Tanzania na Namibia zote zinaongozwa na Marais wanawake, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Netumbo Nandi-Ndaitwah. Uongozi wao unatazamwa kama ishara ya maendeleo ya uongozi shirikishi barani Afrika.
