Addis Ababa. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inachukua hatua za kimkakati za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria ikitazamia kutimiza lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, kama ajenda ya Afrika inavyoelekeza.
Amesisitiza kuwa mapambani dhidi ya malaria si suala la afya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo, uchumi na ustawi wa rasilimali watu barani Afrika na kwamba kufikia malengo yaliyowekwa Afrika inahitaji uongozi na usimamizi thabiti wa Waafrika wenyewe, umiliki wa kweli wa programu zake pamoja na dhamira ya kisiasa ya muda mrefu.
Ametoa rai hiyo wakati akishiriki katika mkutano wa ngazi ya juu na vyombo vya habari uliolenga kujadili ufadhili endelevu wa mapambano dhidi ya malaria barani Afrika, pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Hatua ambazo Tanzania inachukua ni pamoja na kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika tafiti za kisayansi na ubunifu kupitia Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), ikiwemo utafiti wa teknolojia za kisasa za kudhibiti maambukizi ya malaria.
Amebainisha jitihada za Tanzania za kuongeza matumizi ya vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu wanaoeneza malaria, chanjo za malaria, pamoja na kuboresha mifumo ya matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa kama miongoni mwa njia zilizotumika.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ni mwenyeji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA) kama taasisi ya kuratibu mapambano hayo barani Afrika, iliyojengwa juu ya mifumo madhubuti ya uwajibikaji, pamoja na uwezo wa utekelezaji unaolenga matokeo.
Ametumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, akieleza kuwa pamoja na jitihada za ndani, taasisi za kimataifa na washirika wa maendeleo wanapaswa kutekeleza ahadi zao kikamilifu na kwa wakati, hususan katika kuimarisha Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Malaria (The Global Fund) pamoja na matumizi ya rasilimali za Benki ya Dunia kwa ajili ya programu za malaria.
