Home HabariTanzania, Uganda zasaini makubaliano kuifanya Tanga kitovu cha nishati kikanda

Tanzania, Uganda zasaini makubaliano kuifanya Tanga kitovu cha nishati kikanda

by Joshua Kiziba

Dar es Salaam. Tanzania na Uganda zimesaini Hati ya Makubaliano ya kuiendeleza Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda, katika hafla iliyofanyika Agosti 6, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam. Utiaji saini huo ulishuhudiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi.

Makubaliano hayo yanahusisha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na kampuni ya biashara ya mafuta na nishati ya Vitol Bahrain E.C. Kabla ya hafla hiyo, Rais Samia na Rais Museveni walifanya mazungumzo ya ana kwa ana Ikulu.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mpango huo unalenga kutumia nafasi ya kimkakati ya Tanga na miundombinu iliyopo ya usafirishaji wa nishati ili kuufanya mkoa huo kuwa kitovu muhimu cha nishati katika ukanda.

Kwa mujibu wa Ndejembi, utekelezaji wa makubaliano hayo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kiuchumi, kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya nishati na kuongeza mchango wa Afrika Mashariki katika biashara ya nishati. Amesema pia yanaonesha dhamira ya nchi za Afrika kushirikiana kupanga, kufadhili na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Monica Masanza, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika maono ya muda mrefu ya ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati. Amesema mradi huo unatarajiwa kuchochea ajira kwa vijana, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Tanga pia ni kituo cha mwisho cha Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga. Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, bomba hilo la inchi 24 lina urefu wa kilomita 1,443 na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku kuelekea masoko ya kimataifa.