Home » Tanzania yasajili miradi ya USD bilioni 1 itakayotoa ajira 19,700

Tanzania yasajili miradi ya USD bilioni 1 itakayotoa ajira 19,700

by Joshua Kiziba

Tanzania imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji baada ya kusajili miradi 177 yenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 1.2 katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, miradi ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 19,750 kwa Watanzania.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, wakati wa ufunguzi wa Baraza la kwanza la wafanyakazi wa taasisi hiyo, kufuatia kuunganishwa kwa TIC na EPZA.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, alisisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa TISEZA kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuongeza ufanisi katika kuhudumia wawekezaji, ili kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji wa ndani na nje.

Alibainisha kuwa uwekezaji ni mhimili muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga sekta binafsi kuchangia asilimia 70 ya Pato la Taifa.

Kwa upande wake, Teri alieleza kuwa ushirikiano unaoendelea kati ya TISEZA na Ofisi ya Rais – Uwekezaji una mchango mkubwa katika kukuza uwekezaji endelevu na kuongeza fursa za ajira nchini.