Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema tafiti zinaonesha kuwa kuendesha gari la umeme nchini ni nafuu kwa takribani asilimia 85 kwa kila kilomita ikilinganishwa na gari linalotumia petroli au dizeli. Amesema wastani wa gharama ya gari la mafuta ni karibu shilingi 200 kwa kilomita moja, huku gari la umeme likigharimu takribani Sh25 pekee.
Mramba ametoa kauli hiyo Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa matumizi ya magari ya umeme nchini kupitia kampuni ya DOW ELEF AUTO EV (ZERA) Limited.
Amesema tofauti hiyo ya gharama inaonesha wazi kuwa teknolojia ya magari ya umeme ni nafuu zaidi na inaweza kusaidia wananchi kupunguza matumizi katika sekta ya usafiri.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi ya sekta ya usafiri nchini na inaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kukuza uwekezaji na kuhamasisha matumizi ya teknolojia safi ya nishati.
Mramba amesema Serikali tayari imeweka mazingira wezeshi kwa kupitisha Mfumo wa Kitaifa wa Sera ya Magari ya Umeme (National Electric Vehicles Policy Framework) Desemba 2024, unaolenga kuhamasisha uzalishaji na matumizi ya magari ya umeme, kuunganisha sekta hiyo na nishati jadidifu pamoja na kujenga miundombinu ya vituo vya kuchaji.
Aidha, amesema Tanzania imeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme hadi zaidi ya megawati 4,500 na upatikanaji wa umeme umefikia asilimia 85.5 mwaka 2025. Afrika kwa sasa ina zaidi ya magari ya umeme 30,000, huku Tanzania ikikadiriwa kuwa na zaidi ya 10,000, zikiwemo pikipiki za magurudumu mawili na matatu.
Kampuni ya DOW ELEF AUTO EV (ZERA) Limited imeanza kwa kuagiza magari kamili ya umeme na inapanga baadaye kuanza kuyaunganisha nchini pamoja na kuanzisha kiwanda kitakachochochea ajira na ujuzi kwa vijana.
