Home » Umoja wa Mataifa waipongeza Tanzania kwa kuwa mfano wa amani Afrika

Umoja wa Mataifa waipongeza Tanzania kwa kuwa mfano wa amani Afrika

by Joshua Kiziba

Addis Ababa. Umoja wa Mataifa (UN) umeipongeza Tanzania kwa historia yake ya amani na uthabiti, akieleza kuwa, “Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani barani Afrika,” na kutambua juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mifumo ya taasisi na utatuzi wa changamoto kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.

Hayo yameelezwa na Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed akiwasilisha salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kwa Rais Samia walipokutana kuzunguma jijini Addis Ababa, Ethiopia. Mazungumzo hayo yamegusia mageuzi ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, ushiriki wa vijana katika maendeleo, na umuhimu wa kuimarisha uratibu kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia ameeleza dhamira ya Tanzania katika kuendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kiutawala, pamoja na kuimarisha ushirikiano na UN katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi wengi ikiwemo afya, elimu, maji safi, usafi wa mazingira, na kupunguza umaskini.

Aidha, amepongeza na kuthamini mchango wa Umoja wa Mataifa na taasisi zake katika jitihada za pamoja za maendeleo nchini, hususan katika nyanja za ushirikiano wa kidiplomasia na msaada wa maendeleo katika sekta mbalimbali.

Pia, ameonesha utayari wa Serikali katika kumpokea mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa aliyeomba kuja nchini kwa ajili ya kuwasilisha ujumbe maalum wa Katibu Mkuu wa UN.