Dar es Salaam. Wakati Watanzania na raia wa kigeni wakijiandaa kushuhudia Tamasha la Kizimkazi 2026, swali linalojitokeza kwa wengi ni nini hasa kinacholifanya eneo hili la Kusini mwa Unguja kuwa na mvuto wa kipekee unaovuka mipaka ya Zanzibar?
Zaidi ya kuwa mwenyeji wa tamasha hilo, Kizimkazi ni hazina inayobeba historia ya karne nyingi, utamaduni wa Waswahili na fursa kubwa za utalii pamoja na uchumi wa buluu.
Kizimkazi inajulikana kwa mandhari yake ya asili, fukwe zenye kuvutia na ukaribu wake na Bahari ya Hindi. Mazingira hayo ni sehemu muhimu ya maisha ya jamii ya eneo hilo, yakichochea shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, thamani ya Kizimkazi haipo katika uzuri wa mazingira yake pekee, bali pia katika nafasi yake kama eneo lenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mchanganyiko wa historia, utamaduni, rasilimali za bahari na vivutio vya utalii umelifanya Kizimkazi kuwa eneo lenye fursa pana za uwekezaji, ajira na biashara kupitia utalii na uchumi wa buluu.
Urithi wa karne nyingi
Historia ya Kizimkazi ina mizizi ya karne nyingi. Ushahidi wa maandishi ya kale unaonyesha kuwa Kisiwa cha Unguja kilikuwa kikijulikana na kikiwa sehemu ya safari na biashara za baharini tangu zamani.
Miongoni mwa maandishi hayo ni Periplus of the Erythraean Sea, yaliyoandikwa takribani karne moja baada ya kuzaliwa Kristo, ambayo yanaeleza maeneo mbalimbali yaliyokuwa yakifikiwa na wafanyabiashara katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Hata hivyo, historia ya Kizimkazi haijengwi na ushahidi wa vitabuni pekee. Eneo hilo pia linajulikana kutokana na uwepo wa Msikiti wa Kizimkazi uliopo Dimbani, ambao ni miongoni mwa alama muhimu za urithi wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi, msikiti huo ulijengwa mwaka 1107 na Sheikh Al Sayyid Abu Imran Mussan bin Muhammad. Kinachoufanya kuwa wa kipekee ni ukweli kwamba, licha ya kuwa na historia ya zaidi ya miaka 800, bado unatumiwa hadi leo.
Msikiti huo una maandishi ya Kiarabu ya mtindo wa Kufi, ambayo ni ushahidi mwingine wa historia ya kuenea kwa Uislamu Zanzibar tangu karne nyingi zilizopita.

Muundo wa ujenzi wake unaotumia matumbawe ya baharini, mchanganyiko wa usanifu wa Kiswahili na Kiarabu pamoja na mimbari ya kale, ni sehemu ya mvuto unaowafanya wageni kuendelea kuutembelea.
Historia hii ya Kizimkazi inaonyesha kuwa kabla hata ya Wareno kufika Afrika Mashariki katika karne ya 15, Zanzibar na ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki ulikuwa tayari sehemu ya biashara iliyowaunganisha watu kutoka India, Uajemi na maeneo mengine ya Asia.
Vivutio vya baharini
Bahari inayolizunguka Kizimkazi imeendelea kuwa moja ya sababu kuu zinazolifanya eneo hilo kuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Miongoni mwa vivutio vinavyotambulika zaidi ni uwepo wa pomboo (dolphins) ambao wamekuwa sehemu ya utambulisho wa eneo hilo na kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika tasnia ya filamu na utalii, mara nyingi picha za watu wakiwa wanaogelea na pomboo huonekana kama uzoefu unaopatikana maeneo ya mbali duniani, lakini ukweli ni kwamba viumbe hao hupatikana kwa wingi katika bahari inayozunguka Kusini mwa Unguja.

Fukwe murua za Kizimkazi pia zimekuwa kivutio kikubwa kwa uwekezaji wa utalii, hasa ujenzi wa hoteli na huduma zinazowawezesha wageni kufurahia mandhari ya Bahari ya Hindi.
Vyakula, utamaduni
Mbali na historia na vivutio vya baharini, Kizimkazi ni sehemu inayobeba utamaduni wa Pwani ya Waswahili.
Mila na desturi za wakazi wake zimeathiriwa na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali zikiwamo za Washirazi, Waarabu, Wahindi, Waswahili na dini ya Kiislamu.
Vyakula kama mihogo, samaki na wali ni sehemu ya utambulisho wa maisha ya watu wa eneo hilo, huku wakazi wake wakifahamika kwa ukarimu na uungwana unaowavutia wageni.
Faida kwa Tanzania
Kama ilivyo kwa maeneo mengine yenye historia yakiwamo Kilwa, Bonde la Ngorongoro na Pate, Kizimkazi ni mojawapo ya maeneo muhimu katika dhana ya utalii wa urithi.
Utalii wa urithi hauhusishi tu kutembelea vivutio vya asili, bali pia kujifunza historia ya watu, maisha yao, tamaduni zao na namna walivyohifadhi utambulisho wao kwa vizazi mbalimbali.
Watalii wanaoongezeka katika maeneo ya aina hii hutoa fursa kwa sekta mbalimbali kama hoteli, usafiri na huduma nyingine za wageni, huku mapato yakiongezeka kwa jamii na nchi kwa ujumla.
Faida nyingine ni utalii wa urithi unaojenga fahari kwa wananchi kuhusu historia na utambulisho wao. Kujua kwamba jamii imekuwapo kwa miaka mingi na imeendelea kuhifadhi urithi wake ni sehemu ya kujenga uzalendo.
Kizimkazi ni muhimu kwa Tanzania kwa namna zaidi ya moja. Ni sehemu inayochangia katika sekta ya utalii, kutoa fursa za biashara, kukuza uchumi wa buluu na kuwakutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali.
