Home » Uwanja wa Sumbawanga wakamilika, safari zaanza rasmi

Uwanja wa Sumbawanga wakamilika, safari zaanza rasmi

by Joshua Kiziba

Rukwa: Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amewataka wananchi kutumia vyema fursa zinazotokana na maboresho ya sekta ya uchukuzi kujikwamua kiuchumi kwa kuibua na kuendeleza miradi ya kimkakati.

Kihenzile ametoa kauli hiyo alipozindua Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga mkoani Rukwa na kueleza kuwa uwanja huo ni kichocheo muhimu cha maendeleo kwa wananchi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya uchukuzi ili kuinua maisha ya Watanzania.

Katika tukio hilo, ndege ya abiria ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ilitua kwa mara ya kwanza na kupokewa kwa “water salute”, kuashiria kuanza rasmi kwa huduma za usafiri katika kiwanja hicho.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Makongoro Nyerere, amesema uzinduzi wa kiwanja hicho utafungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo.

Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo, akiwemo Mikidadi Machesha, msafiri wa kwanza kutoka Sumbawanga kwenda Dar es Salaam, aliyesema usafiri wa anga utarahisisha safari na kupanua wigo wa ajira.

“Zamani tulisafiri zaidi ya kilomita 1,148 hadi Dar es Salaam, lakini sasa ni saa moja na dakika 40 tu,” amesema Machesha.

Ameiomba mamlaka ya usafiri kuhakikisha kunakuwa na safari za kila siku, akibainisha kuwa uwanja huo ni lango muhimu la usafiri kwa mikoa ya jirani na nchi kama Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Abdul Mwondokaleo amesema uwanja huo una uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 150,000, huku akibainisha kuwa katika kipindi cha mwanzo kutakuwa na nauli nafuu ili kuwavutia wasafiri.

Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga umegharimu zaidi ya Sh60 bilioni hadi kukamilika kwake.