Home » Wakaguzi waridhishwa na ubora wa Bwawa la Julius Nyerere

Wakaguzi waridhishwa na ubora wa Bwawa la Julius Nyerere

by Joshua Kiziba

Pwani: Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) imekagua maendeleo ya uzalishaji wa umeme katika hilo na kuridhishwa na usimamizi pamoja na utekelezaji wake, uliokidhi viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali.

“Tumeridhishwa na jinsi mradi huu ulivyosimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Ukilinganisha na miradi mingine barani Afrika, mradi huu umejengwa kwa ubora wa hali ya juu na umeleta unafuu katika huduma ya umeme nchini. Haya ni mafanikio makubwa kwa taifa,” alieleza Mwenyekiti wa Kamati, Dkt. Jim Yonazi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Petro Lyatuu, amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na mchango wake tayari umeanza kuonekana.

Amefafanua kuwa mwaka 2021, gridi ya taifa ilikuwa na jumla ya megawati 1,600, lakini kwa sasa uwezo wa uzalishaji umefikia zaidi ya megawati 4,000, zaidi ya mara mbili ya kiwango cha awali.

Katika hitimisho la ziara hiyo, kamati imeeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya umeme unaifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji na kitovu cha usambazaji wa umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.