Dar es Salaam. Wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China ukiendelea kuzalisha fursa nyingi za kiuchumi, imeelezwa kuwa baadhi ya Watanzania wanashindwa kunufaika kikamilifu na fursa hizo kutokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuepukika.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kutofahamu au kutofuata sheria na taratibu za usafirishaji wa bidhaa, uzalishaji mdogo wa bidhaa zinazohitajika katika soko la China, kushindwa kuongeza thamani ya bidhaa, matumizi ya vifungashio visivyokidhi viwango, pamoja na ukiukwaji wa baadhi ya sheria za nchi hiyo.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Juni 25, 2026, na Balozi wa Tanzania nchini China, Dk. Suleiman Haji Suleiman, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk. Suleiman amesema kwa sasa Tanzania inauza bidhaa zenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.8 (Sh trilioni 4.7) katika soko la China, kiwango kinachowakilisha chini ya asilimia 10 ya biashara yote kati ya nchi hizo mbili. Kwa upande mwingine, bidhaa zinazoagizwa kutoka China zina thamani ya zaidi ya dola bilioni 21.3 (Sh trilioni 55.9).
“Tunaona kuna pengo kubwa katika mizania ya biashara. Wenzetu wanauza bidhaa nyingi kwetu kuliko tunavyouza kwao, jambo linaloonyesha bado hatujatumia kikamilifu fursa zilizopo katika soko la China,” amesema.
Amefafanua kuwa uzalishaji usiotosheleza wa bidhaa zinazohitajika nchini China na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu namna ya kuwafikia wanunuzi wa soko hilo ni miongoni mwa sababu zinazowakwamisha wafanyabiashara wa Kitanzania.
Aidha, amesema baadhi ya wafanyabiashara hawafahamu taratibu za kusafirisha bidhaa wala namna ya kupata vibali vinavyohitajika nchini China, hali inayosababisha bidhaa zao kukwama bandarini.
“Suala la vifungashio pia ni changamoto. Baadhi ya watu husafirisha bidhaa kama korosho zikiwa zimefungashwa kwenye magunia, jambo linalopunguza thamani na ushindani wa bidhaa hizo katika soko la China,” amesema.
Pamoja na changamoto hizo, Dk. Suleiman amesema bidhaa za Tanzania zinazoendelea kuwa na mahitaji makubwa nchini China ni pamoja na parachichi, korosho, ufuta, katani, tumbaku, karafuu na mazao mengine ya kilimo. Amesisitiza kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni ikiwa wazalishaji wataongeza uzalishaji wenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Katika sekta ya utalii, amesema idadi ya watalii kutoka China imeongezeka kwa kasi baada ya uzinduzi wa filamu ya Amazing Tanzania, ikipanda kutoka watalii 14,000 mwaka 2022 hadi kufikia 82,000 mwaka huu.
Kwa upande wa elimu, amesema China inaendelea kutoa ufadhili wa masomo pamoja na mafunzo ya muda mfupi katika teknolojia ya Akili Bandia (AI) kwa vijana wa Kitanzania.
Dk. Suleiman amesema Ubalozi wa Tanzania nchini China umejipanga kuhakikisha unatoa huduma kwa Watanzania wote wanaotaka kuingia katika soko la China bila ubaguzi.
“Si vyema kufika ubalozini pale tu unapopata tatizo. Wananchi wanaweza pia kufika kupata ushauri kuhusu fursa mbalimbali zilizopo. Ubalozi uko tayari kuwahudumia Watanzania wote bila kujali uwezo wao au ukubwa wa biashara zao. Kazi yetu ni kuhakikisha wanapata taarifa, mwongozo na usaidizi unaohitajika ili waweze kutumia fursa zilizopo nchini China,” amesema.
Ameongeza kuwa wananchi watakaotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) watapata fursa ya kupata maelezo kuhusu biashara, uwekezaji na taratibu za kupeleka bidhaa zao katika soko la China.
Aidha, amewahimiza wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani kutumia vyema uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China kwa kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuzingatia viwango vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza pengo la biashara kati ya nchi hizo mbili na kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Dk. Suleiman pia amekumbusha kuwa kuanzia Mei 1, 2026, China ilianza rasmi kutekeleza sera ya kuondoa ushuru wa forodha (zero tariff) kwa bidhaa kutoka Tanzania na nchi nyingine 52 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na taifa hilo.
Amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa imefungua soko la watu zaidi ya bilioni 1.4 nchini China kwa bidhaa za Afrika bila kutozwa ushuru wa forodha, hivyo kutoa fursa kubwa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kuongeza mauzo yao katika soko hilo.
