Home ยป Tanzania yatimiza maono ya Mwalimu Nyerere ya kuwa na Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa
Makao-Makuu-Ulinzi-wa-Taifa

Tanzania yatimiza maono ya Mwalimu Nyerere ya kuwa na Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa

by Joshua Kiziba

Tanzania leo imeandika historia kubwa ambapo kwa mara ya kwanza imekuwa na Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, ambapo ni ofisi za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ofisi za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa zitakazokuwa sehemu moja jambo ambalo ni muhimu katika kuimarifa ufanisi wa kazi.

Jengo hilo lililozinduliwa leo Kikombo mkoani Dodoma limehitimisha safari iliyoanza mwaka 1964 ambapo wazo la kuwa na Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa lilitolewa wakati jeshi hilo likiundwa.

Safari hiyo iliendelea na miaka 10 baadaye, mwaka 1974, wazo la kuwa na Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa liliingizwa kwenye Mpango Kazi wa jeshi. Kutokana na changamoto za kifedha na Vita vya Kagera, jengo hilo halikujengwa na ilipofika mwaka 2014 ilipitishwa kuwa lijengwe ilipo Kambi ya Lugalo, Dar es Salaam, na jiwe la msingi liliwekwa tayari ujenzi kuanza.

Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, mpango wa serikali kuhamia Dodoma ukapata msukumo mpya, hivyo ikaelekezwa kuwa jengo hilo lijengwe Dodoma. JWTZ ilihamia Dodoma na kuwa ofisi za muda Msalato, huku wizara ikiwa katika Mji wa Serikali.

Mwaka 2019, Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hizo katika Kijiji cha Kikombo, na ujenzi ulianza rasmi mwaka 2020.

Miaka sita baadaye tangu kuanza kwa ujenzi, na miaka 62 tangu kutolewa kwa wazo hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo amezindua awamu ya kwanza ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa ambayo imejengwa na watalaamu wa ndani kwa thamani ya shilingi bilioni 121 (majengo, miundombinu na samani).

Akifungua jengo hilo Dkt. Samia amesema uwekezaji katika miundombinu ya ulinzi ni sehemu ya msingi ya kulinda heshima ya Taifa, amani ya nchi na mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi na ametaka ofisi hizo zitumike kama kitovu cha uratibu wa kimkakati, uchambuzi wa kitaalamu na usimamizi wa kisasa wa shughuli za ulinzi wa Taifa.

Awamu ya pili na ya tatu zitakazohusisha ofisi na majengo ya makazi zinatarajiwa kuanza pindi taratibu za maandalizi zitakapokamilika ambapo zitagharimu shilingi bilioni 107.6 na shilingi bilioni 90.1, mtawalia.